Breaking News

Mechi 5 kali SIMBA na MTIBWA Jamhuri

Timu ya Simba imebanwa mbavu na kutoka sare ya bila kufunga na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro. Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha jumla ya pointi 45 na Mtibwa ikiwa na pointi 31.
Kwa kawaida mechi kati ya Simba na Mtibwa huwa ni ngumu na zenye upinzani mkali na hasa zile zinazochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Mtibwa kutumia Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro. Lakini inapocheza dhidi ya timu kubwa mbili, Simba na Yanga, timu hiyo inautumia uwanja huo kuwa wa nyumbani.
Rekodi zinaonyesha kuwa katika mechi tisa ambazo timu hizo zilikutana tangu msimu wa 2007/08, Simba imeshinda mechi tano, Mtibwa ikishinda mbili na zikitoka sare mara tatu kwenye uwanja huo.
Zifuatazo ni mechi tano kali za Ligi Kuu ambazo zilichezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
1. Mtibwa 1-3 Simba (2007/08)
Ilikuwa ni Oktoba 7, 2007, msimu wa Ligi Kuu 2007/08, Mtibwa ilipoambulia kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Simba nyumbani. Yalikuwa ni mabao ya Nico Nyagawa na Mkenya, Moses Odhiambo aliyefunga magoli mawili.
2. Mtibwa 1-0 Simba (2008/09)
Ilikuwa moja kati ya mechi ya kusisimua kwenye Uwanja wa Jamhuri iliyochezwa Machi 22, 2009.
Ilikuwa ni mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu 2008/09, Simba ikaangukia pua kwa kuchapwa bao 1-0.
Bao pekee kwenye mchezo huo lilifungwa na Omari Matuta, dakika ya 39, lililosimama hadi mwisho wa mechi hiyo.
3. Mtibwa 0-4 Simba (2009/10)
Msimu uliofuata, Simba ilikwenda tena kwenye Uwanja wa Jamhuri ikiwa na kidonda cha kufungwa bao 1-0. Kwa hasira, iliangusha kipigo kikali cha mabao 4-0 dhidi ya wenyeji wao, Mtibwa Sugar.
Mechi ilichezwa Aprili 21, 2010, ikiwa ni ya mzunguko wa pili msimu wa 2009/10. Wafungaji kwenye mechi hiyo walikuwa ni Mussa Hassan Mgosi aliyefunga magoli mawili kwenye mechi hiyo. Mohamed Kijuso alifunga bao moja, pamoja na Ramadhani Chombo ‘Redondo’.
4. Mtibwa 1-2 Simba (2011/12)
Simba iliendelea kuitesa Mtibwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, kwani msimu wa 2011/12 ilikwenda tena Morogoro na kuichapa mabao 2-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Machi 18, 2012, mabao ya washindi yalifungwa na Patrick Mafisango (marehemu) na Mzambia Felix Sunzu, huku la kufutia machozi la Mtibwa likifungwa na Hussein Javu.
5. Mtibwa 2-0 Simba (2012/13)
Baada ya misimu mitatu kupita, hatimaye Mtibwa ilizinduka msimu wa 2012/13 na kuichakaza Simba mabao 2-0. Mzaha wa kipa Juma Kaseja ndiyo ulioiponza Simba kwenye mechi hiyo ya Novemba 4, 2012.
Mzaha wa kwanza ulisababisha Mohamed Mkopi kufunga bao la kwanza dakika ya 34. Wakati mastraika na Simba hakipigana kuhakikisha wanapata japo bao la kusawazisha, mzaha mwingine wa kutaka kumpiga chenga Hussein Javu, ulisababisha kunyang’anywa mpira huo na straika huyo akaujaza wavuni, dakika moja tu kabla ya mechi kumalizika.

No comments