Breaking News

SIMBA KUFUATA BARAKA ZA WABUNGE WAO DODOMA KABLA YA KUWAVAA SINGIDA

NA ZAITUNI KIBWANA

 

 

KIKOSI cha Simba kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kesho kwenda mkoani Singida tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida United, huku wakipanga kuweka vituo katika mikoa ya Morogoro na Dodoma.

Singida United ambao ndio mwenyeji wa mchezo huo, watawakaribisha Simba kwenye Uwanja wa Namfua, mjini humo Jumapili, huku Wekundu wa Msimbazi hao wakiwa na matumaini ya kutawazwa kuwa mabingwa iwapo watashinda mchezo huo.

Simba wamefikisha pointi 65 hivyo wanahitaji pointi mbili tu kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu Bara, waliokuwa wakiusotea bila mafanikio tangu msimu wa 2011/12.

Kama Simba watashinda mchezo huo dhidi ya Singida United, sherehe za ubingwa zitaanzia huko kwani hakuna timu yoyote inayoweza kufikia pointi 68 watakazofikisha, wakiwamo mabingwa watetezi, Yanga ambao kwa sasa wana pointi 48 wakiwa wamebakiza mechi sita.

Kama watashinda mechi hizo zote, Wanajangwani hao watafikisha pointi 66 ambazo zitakuwa zimeshapitwa na Simba.

Akizungumza na BINGWA jana kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini kwa madai kuwa si msemaji wa klabu hiyo, mmoja wa viongozi wa juu wa Simba, alisema kuwa mchezo wao huo ujao wanauwekea mikakati kabambe ili washinde.

Alisema kuwa benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Mfaransa Pierre Lechantre na msaidizi wake, Masoud Djuma raia wa Burundi, limekuwa likiandaa kila aina ya mbinu kuhakikisha wanashinda mchezo huo muhimu mno kwao.

“Hatujajua bado tuweke kituo Dodoma au Morogoro, ila timu itasimama kote huko kabla ya kuendelea na safari…kwa sasa akili zetu zipo Singida United ambapo tuna imani mchezo utakuwa mgumu,” alisema.

Alisema watakapokuwa Dodoma, watapata fursa ya kukutana na wabunge ambao ni wapenzi wa Simba ili kupata baraka zao kabla ya kuvamia Singida.

 

Kwa upande wake, Djuma amesema hawatabweteka na ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Ndanda FC na badala yake, watahakikisha wanapambana ili kushinda michezo yao yote iliyobakia.

“Nadhani michezo iliyobaki ndio mibaya zaidi maana unaweza kufanya kosa kidogo tu mwenzio aliye nyuma yako akakuzidi ujanja, ndiyo maana nasema hapa hakuna kulala mpaka mwisho,” alisema Djuma.

Simba mara ya mwisho walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011/12 na tangu wakati huo, wamekuwa wakilisotea taji hilo bila mafanikio, wakiwakodolea macho watani wao wa jadi, Yanga, wakijinafasi na ‘mwali’ mara nne na Azam mara moja.

No comments