SAFU YA USHAMBULIAJI STEND YA MVURUGA KOCHA
BAADA ya kutinga robo fainali ya michuano ya Uhai Cup, Kocha wa Stand United, Athumani Bilali “Bilo” amesema bado ana kazi nzito ya kuhakikisha safu yake ya ushambuliaji inakuwa imara kwani bila kufanya hivyo hawatoweza kufika mbali kwenye ligi hiyo.
Stand United imetinga robo fainali hiyo sambamba na Simba kutoka kundi B, huku Chama la Wana likiwa limeweka rekodi ya kutopoteza mchezo wowote kwenye mechi tatu walizocheza.
Kocha Bilo alisema bado kuna mapungufu makubwa katika safu ya Ushambuliaji imekuwa butu ambapo amesema kwa muda uliobaki ni lazima wayafanyie kazi haraka ili kikosi kiwe bora zaidi.
“Lazima niseme ukweli bado nina kazi ya kurekebisha makosa kwenye safu ya ushambuliaji inakosa umakini inapofika langoni angalia mchezo wetu na Simba tulikosa mabao ya wazi kabisa hili halikubaliki,” alisema Bilo.
Hata hivyo Kocha huyo alisema mipango yao ni kutwaa ubingwa huo ambapo amewataka mashabiki wa chama hilo kuandaa sherehe za ubingwa kwani lazima warudi Shinyanga na Taji hilo.
“Tutaanza robo fainali na Ndanda kisha tukiwatoa tutakuwa tunajipanga kwa ajili ya nusu na hatimaye fainali haya mapungufu nitayafanyia kazi mipango yetu ni kunyakuwa taji hili msimu huu,” alisema Kocha huyo.
Ligi hiyo inayochezwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dodoma hadi sasa imefikia katika hatua ya Robo fainali ambapo ilianza na timu 16 za Ligi Kuu na sasa zimebakia nane pekee.
No comments