WACHEZAJI BORA WA KILA NAMBA ZA JEZI WALIOPO URUSI 2018
KWENYE fainali za Kombe la Dunia huko Russia kuna timu 32. Kila timu moja imetakiwa kuwa na wachezaji 23 kwenye kikosi chake, ambao watahusika kwenye fainali hizo.
Kwa maana hiyo basi, hata namba za jezi zitakazoonekana kwenye fainali hizo kwa wachezaji zitaanzia 1 hadi 23. Kutokana na hilo, Mwanaspoti linakuletea mchezaji bora kwa kila namba ya jezi waliopo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia.
1.David De Gea (Hispania)
Hakuna ubishi, kwa wachezaji wote kutoka vikosi 32 vilivyopo Russia ambao wanavaa jezi yenye namba 1 mgongoni, hakika Mhispaniola, David De Gea ndiye bora zaidi yao. Sawa, kipa huyo alifanya makosa kwenye mechi ya kwanza ya La Roja dhidi ya Ureno, lakini hilo haliondoi ukweli kwamba De Gea ndiye mchezaji bora anayevaa jezi namba 1 kwenye fainali hizo.
2.Toby Alderweireld (Ubelgiji)
Tayari imeshuhudiwa wachezaji kadhaa wanaovaa jezi namba 2 mgongoni kwenye fainali hizo, lakini asikwambie mtu, Toby Alderweireld, ndiye mchezaji bora kati ya wale waliopo kwenye fainali hizo za Russia ambao jezi zao zimeandikwa namba 2 mgongoni.
Toby anakipiga kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur na siku za karibuni amekuwa akihusishwa na Manchester United.
3.Gerard Pique (Hispania)
Si jina dogo kwenye soka. Huduma yake anayotoa huko Barcelona na kwenye kikosi cha Hispania haina mashaka. Pique yupo kwenye fainali za Kombe la Dunia na anavaa jezi yenye namba 3 mgongoni.
Kwa wachezaji wenye jezi zenye namba 3 kwenye fainali hizo za Russia, hakika Pique ndiye anayetajwa kuwa bora zaidi miongoni mwao.
4.Raphael Varane (Ufaransa)
Varane ni mmoja kati ya mabeki bora kabisa wa kati duniani kwa sasa. Staa huyo wa Real Madrid yupo kwenye fainali za Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ufaransa, ambako anavaa jezi namba 4. Ukweli kwenye orodha ya wachezaji waliopo kwenye fainali hizo za Russia, wenye jezi yenye namba hiyo wengi ni mahiri, lakini Varane ni mahiri zaidi kulinganisha na wengine.
5.Sergio Busquets (Hispania)
Kiungo wa kati mkali kabisa kwenye soka hili la kizazi cha kisasa. Busquets yupo kwenye fainali za Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Hispania na hakika kwenye orodha ya wachezaji wote waliopo kwenye fainali hizo ambao wanavaa jezi namba 5, Mhispaniola huyo, Busquets ni bora zaidi na hata thamani yake ipo juu pia.
6.Andres Iniesta (Hispania)
Kama unavaa jezi namba 6 na upo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, basi namba hiyo inalingana na ile anayovaa fundi wa mpira duniani, Andres Iniesta. Kwa maana hiyo, kuna wachezaji 32 wanaovaa jezi namba 6 kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, lakini kwenye orodha hiyo yote, Iniesta ndiye mchezaji bora zaidi kwa wale wenye namba 6 mgongoni huko Russia.
7.Cristiano Ronaldo (Ureno)
Kuna mwenye swali kuhusu mchezaji bora kwenye fainali za Kombe la Dunia anayevaa jezi namba 7? Cristiano Ronaldo ndilo jina linalochomoza kwenye orodha hii, hasa ikiwa staa huyo wa Ureno tayari ameshafanya mambo yake akifunga hat-trick kwenye mechi ya kwanza huko Russia. Lakini, haikuwa tu kupiga hat-trick, bali amewafanyia hivyo Hispania mbele ya mabeki wake wakorofi.
8.Toni Kroos (Ujerumani)
Wapo wachezaji wengi sana wenye jezi namba 8 mgongoni ambao wanakipiga kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea huko Russia, lakini hakuna ubishi kiungo matata wa Kijerumani, Toni Kroos, ndiye mkali wao. Kroos ni mmoja kati ya wachezaji muhimu kabisa kwenye kikosi cha Ujerumani ambao wapo Russia kupambana kutetea ubingwa ambao waliubeba miaka minne iliyopita.
9.Robert Lewandowski (Poland)
Kuna kocha ambaye atakataa kumchukua Lewandowski kwenye kikosi chake akacheze namba 9? Kwenye fainali za Russia 2018 kuna mastaa 32 wenye jezi namba 9, miongoni mwao ni Lewandowski, ambaye kimsingi ndiye mchezaji bora zaidi kwenye orodha ya wakali hao wanaovaa jezi hiyo ya kutupia wavuni waliopo kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia.
10.Lionel Messi (Argentina)
Kama unavaa jezi Namba 10 na upo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia lazima utakuwa na ufahamu tu kwamba kuna mtu aliyekuwa bora zaidi anavaa namba hiyo pia. Ni Lionel Messi wa Argentina. Sawa, alishindwa kuipa ushindi timu yake kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Iceland kwa kukosa mkwaju wa penalti, lakini ukweli, jezi namba 10 katika watu waliowahi kuvaa Messi ndiye bora zaidi.
11.Philippe Coutinho (Brazil)
Fundi wa mpira kutoka Brazil, Coutinho atakuwapo Russia na kikosi chake cha Brazil ikijaribu kuwania taji lake la tano la ubingwa wa dunia.
Kwenye fainali hizo, Coutinho atakuwa na jezi namba 11 mgongoni, huku kukiwa na wachezaji wengine 31 wenye jezi kama hiyo. Lakini, yote kwa yote, Coutinho anabaki kuwa mchezaji mahiri zaidi anayevaa jezi hiyo kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia 2018.
12.Marcelo (Brazil)
Beki wa kushoto mwenye ujuzi wa kushambulia kama winga vile. Mbrazili, Marcelo anayekipiga kwenye kikosi cha Real Madrid naye atakuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia akiwa na uzi wa wacheza samba, Brazil.
Jezi ya Marcelo itakuwa na namba 12 mgongoni na hivyo kuwa mmoja watakaovaa hiyo namba. Kulinganisha na wengine wote 31, Marcelo ndiye bora zaidi kwenye namba hiyo.
13.N’Golo Kante (Ufaransa)
Mashabiki wake wanakwambia Kante anakaba hadi kivuli. Pengine hilo ndilo linalomfanya Kante kuwa maarufu zaidi kwenye soka la kisasa kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa sana katika kukaba.
Kwa wachezaji waliopo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia jezi ya Kante ni namba 13 na hakika ndiye mchezaji bora zaidi kwa wale wanaotupia uzi wenye namba kama hiyo huko Russia.
14.Cesar Azpilicueta (Hispania)
Huduma yake imekuwa haina shaka kabisa huko Chelsea. Jambo hilo limemfanya ajumuishwe kwenye kikosi cha Hispania kilichopo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia na kukabidhiwa jezi namba 14. Azpilicueta ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa ndani ya uwanja na hakika kama kuna wachezaji mahiri wanaovaa jezi 14 waliopo huko Russia, basi Mhispaniola huyo ni zaidi yao.
15.Sergio Ramos (Hispania)
Bonge la beki la kati. Ukiwa naye kikosini unakuwa na uhakika kuna usalama mkubwa. Ramos naye yupo Russia akiwa na kikosi cha Hispania, ambako amekabidhiwa jezi yenye namba 15. Ramos ni miongoni mwa wachezaji 32 wenye jezi yenye namba hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa mwaka huu, lakini hakuna anayepinga kwamba kwenye orodha ya wote hao, yeye ndiye bora zaidi.
16.Antonio Rudiger (Ujerumani)
Sababu moja iliyomfanya Rudiger kuitwa kwenye kikosi cha Ujerumani ni uwezo wake wa kukaba na kuanzisha mashambulizi. Beki huyo wa Chelsea huko Russia amekabidhiwa jezi yenye namba 16 mgongoni. Wapo wachezaji wengine 31 wenye namba kama hiyo ya jezi, lakini hakuna ubishi, Rudiger anapiku wengine wote kwa ubora katika orodha ya wale waliopo huko Russia kupigania ubingwa wa dunia.
17.Fernandinho (Brazil)
Panga pangua, Pep Guardiola alikuwa hathubutu kumweka benchi kiungo huyo wa Kibrazili huko Manchester City.
Huduma yake bora ya msimu uliopita imemfanya ajumuishwe kwenye kikosi cha Brazil kilichopo huko Russia na kukabidhiwa jezi yenye namba 17. Wapo wengi wanaovaa jezi kama hiyo huko Russia, lakini Fernandinho anafunika wote kutokana na ubora wake.
18.Joshua Kimmich (Ujerumani)
Anatajwa kuwa silaha kubwa kwenye kikosi cha Ujerumani katika fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia. Kimmich amekabidhiwa jezi namba 18, ambayo pia inavaliwa na wachezaji wengine kibao wasiopungua 31, lakini ukweli Mjerumani huyo amekuwa kwenye kiwango bora kabisa na pengine anawaweka wengi benchi kama wangekuwa wanapaswa kuchezea kwenye kikosi kimoja.
19.Sergio Aguero (Argentina)
Tayari ameshatupia mara moja kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia wakati Argentina yake ilipopata sare ya 1-1 na Iceland katika mechi yao ya kwanza. Straika, Aguero uneweza kumwona ndani ya jezi namba 9, lakini staa huyo anavaa jezi namba 19 mgongoni na hakika kwa wachezaji wote wanaovaa namba hiyo huko Russia, Aguero atabaki kuwa kiboko yao.
20.Roberto Firmino (Brazil)
Firmino ni mmoja kati ya wachezaji waliokuwa matata kabisa msimu uliopita kwenye kikosi cha Liverpool. Huduma yake bora imemfanya ajumuishwe kwenye kikosi cha Brazil kilichopo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, ambako amekabidhiwa jezi yenye namba 20. Ni namba inayovaliwa na wachezaji wengine, wasiopungua 31, lakini Firmino ndiye anayeonekana kuwa bora zaidi yao.
21.Edinson Cavani (Uruguay)
Straika wa Uruguay, Edinson Cavani ni mmoja kati ya wachezaji wanaotazamiwa kufanya vyema kabisa katika fainali za Kombe la Dunia huko Russia.
Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa. Kwenye fainali hizo, Cavani amekabidhiwa jezi namba 21, ambayo pia inavaliwa na wachezaji wengine 31.
Hata hivyo, kwenye orodha yote hiyo ya wachezaji wengine, Cavani anabaki kuwa bora zaidi ya wengine.
22.Isco (Hispania)
Fundi wa mpira huyu kutoka Hispania. Ubora wake ulionekana kwenye mechi ya kwanza iliyocheza Hispania dhidi ya Ureno kwenye fainali hizo, ambapo Isco alikuwa akiutaka tu mpira muda wote.
Kwenye kikosi cha La Roja, Isco amekabidhiwa jezi namba 22. Licha ya kwamba jezi hiyo inavaliwa na wachezaji wengi kwenye fainali hizo za Russia, Isco anabaki kuwa bora kwa wote wanaovaa namba hiyo.
23.Davinson Sanchez (Colombia)
Beki wa kati wa Colombia. Kwa msimu uliopita huduma yake aliitoa huko Tottenham Hotspur na kumfanya achaguliwe kuwa mmoja wa mastaa waliopo kwenye fainali za Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Colombia, ambapo amekabidhiwa jezi namba 23. Kwenye fainali hizo, hiyo ndiyo namba ya juu zaidi ambayo inawachezaji 32, lakini kati yao hao, Sanchez yupo vizuri zaidi na kuwa bora wao.
No comments