Breaking News

NIMEWAONA AHLY, VITA CLUB, SIMBA IJIPANGE, KAZI NDIO INAANZA ….







SIMBA wamefanikiwa kuwashinda Waarabu wa Algeria, wameifunga JS Saoura kwa mabao 3-0 na kuongoza Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba wanaongoza kundi lao wakifuatiwa na vigogo, Al Ahly ambao walishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya AS Vita maarufu kama Vita Club ya DR Congo.

Msimamo wa Kundi D, unaonyesha ni Simba wenye pointi tatu, Ahly pointi hizo ila wanazidiwa bao moja, halafu Vita na  Saoura wanashika mkia.

Ndiyo michuano hiyo hatua ya makundi imeanza. Simba inaweka rekodi ya kuwa timu ya Afrika Mashariki kuongoza kundi na itakuwa na wakati mgumu wa kuendelea kubaki hapo.

Mechi ya pili ni ugenini dhidi ya Vita Club ambayo tayari imejeruhiwa ugenini Misri. Timu hiyo imefungwa ikiwa pungufu baada ya mchezaji mmoja kutolewa kwa kadi nyekundu.

Kama Watanzania lazima tukubaliane, kuzipa moyo timu zetu ni jambo namba moja ni jambo sahihi na hii ni kazi yetu. Lakini tunapaswa kuwapa ukweli wa hali halisi.

Ninaamini Simba watakuwa wanajipanga na wana bahati ya kuwa na viongozi wenye uzoefu na michuano ya kimataifa. Lakini lazima wakumbushwe na kuelezwa kilicho sahihi.

Kwa wale waliobahatika kuiona mechi Ahly wakishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Vita Club ninaamini watanielewa zaidi.

Niliingalia mechi hiyo ikirushwa moja kwa moja na ZBC2. Ilicheza baada ya Simba kuwa wamemaliza kazi yao dhidi ya Saoura. Ninaamini benchi la ufundi la Simba lilipata nafasi ya kushuhudia pia.

Mechi ilionyesha wazi kwamba Ahly na Vita Club ni timu nzuri. Ukiangalia mchezo ule unaona Vita Club tayari walipata tatizo la kuwa pungufu na ndilo lililowamaliza. Lakini isingekuwa hivyo, bila shaka Ahly wangekuwa katika wakati mgumu.

Uchezaji wa Vita Club ulionyesha ni timu yenye watu wakomavu hasa katika michuano hiyo. Nilishangazwa maana kabla ilielezwa kuwa wameuza wachezaji kadhaa.

Ukweli ni kwamba wachezaji wake wanaelewana kwa kiwango cha juu na wanajiamini. Walifanya mashambulizi  kadhaa hatari kwenye lango la Ahly ambao walilazimika kufanya kazi ya ziada.

Bila ya ubishi niseme kwamba kwa kiwango cha Saoura, hakiwezi kuwa sawa na Ahly au Vita Club. Maana yake ni hivi, Simba wana mzigo mzito zaidi mbele yao na mechi zao zote mbili zinazofuata ni za ugenini dhidi ya Vita Club halafu Ahly.

Narudia palepale, kwamba Simba wana timu nzuri lakini wanakwenda kukutana na timu nzuri zaidi na zenye uzoefu zaidi.

Tukubali, Saoura hawana uzoefu na uliona hata Simba walipowashambulia sana hawakuwa na mbinu nyingi zinazoonyesha ni wazoefu na wanaweza kupoza mambo kadhaa.

Angalia utaona, hata zile tabia za Kiarabu hazikuwepo kwa asilimia mia. Simba wameitumia nafasi, wamefanya kile kilichotakiwa, safi. Maana tayari wamekusanya pointi tatu kibindoni.

Wakati wakiwa tayari wana mtaji wao kibindoni, tayari mambo sasa ndiyo yanaanza na wajue kazi hata nusu bado.

Unapokutana na timu kama Ahly au Vita Club, mambo yanatakiwa yaende tofauti kabisa. Wao wanajua namna ya kukupa makosa halafu wakuadhibu.

Mfano, uchezaji wa Juuko Murshid. Bila shaka kwa timu kama Ahly au Vita Club angeenda nje mapema sana. Hakuwa makini ukabaji wake ulikuwa unahatarisha “afya” ya Simba katika  mechi hiyo.

Hata mwamuzi wa mchezo huo, pia baadaye alilazimika kutumia nidhamu ya mzazi kumbakiza Juuko uwanjani. Sasa ukikutana na timu ambazo wachezaji wake wanamiliki sana mpira, wanauchezea muda mrefu. Basi lazima suala la ukabaji liwe na nidhamu ya juu sana.

Simba wanaweza kuwafunga Ahly na haitakuwa mara ya kwanza. Lakini lazima wawasome sana na kujifunza mengi. Pia wanaweza kufanya hivyo kwa Vita Club, lakini niwatangulizie maneno haya, itakuwa mechi ngumu ambayo lazima wajipange hasa.

Sherehe za kipigo cha Saoura, zimeisha. Sasa waanze hesabu kwa kuwa muda wenyewe ni mchache, wiki moja kabla ya mechi nyingine huku ukicheza mechi nyingine.



No comments