Breaking News

KOCHA WA SINGIDA UNITED AWAAHIDI UBINGWA MASHABIKI

Arusha. Kocha wa Singida United, Hans Van der Pluijm amesema lengo lake ni kuhakikisha anatwaa ubingwa wa Kombe la FA kama alivyofanya alipokuwa na Yanga.

Singida United na Mtibwa Sugar zitakutana Juni 2 katika fainali ya Kombe la FA itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha na bingwa wa mashindano hayo atapata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mazoezi ya kikosi chake kwenye Uwanja wa Field force ulioko kwa Mrombo nje kidogo ya jiji la Arusha,  kocha Pluijm alisema hii si mara yangu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Kombe FA nilishafanya kwa Yanga hivyo na wapenzi wa Singida wajiandae kupokea kombe.

Alisema ari na moyo walionayo wachezaji wake katika mazoezi anaamini ubingwa tayari ni wao huku akifurahishwa zaidi ya hali ya hewa ya ubaridi ulioko jijini hapa.

“Kwa mazingira ya Arusha na uwanja wa Sheikh Amri Abeid tunakocheza ni dhahiri ni mazingira rafiki kwa soka kwa timu yoyote duniani si Tanzania tu hivyo na mimi nimefurahia hali hii na kikosi changu nao wameanza kuzoea kama ilivyokuwa lengo letu kuwatanguliza mapema.”
Singida United kimeingia Arusha siku 12 kabla ya mchezo huo wa fainali, wakati wapinzani wao Mtibwa Sugar wenyewe wanatarajiwa kuingia wakati wowote kuanzia sasa.

No comments