HIMIDI MAO ATIMKIA PETROJET
Siku moja baada ya Azam FC kukubali ombi lake la kutimukia nje ya nchi Himid Mao Mkami amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Petrojet inayoshiriki Ligi Kuu Misri.
Himid ameitumikia Azam FC kuanzia mwaka 2011, yupo mjini Suez nchini Misri tangu juzi na jana amesaini mkataba kuanza kazi chini ya kocha Hassan Shehata.
Akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa Azam FC, Jaffar Idd alisema ni kweli mchezaji huyo amemalizana na klabu yake mpya tayari kwaajili ya kuitumikia msimu ujao wa ligi.
“Uongozi sisi hatuna kipingamizi, Himid ni mchezaji wetu wa muda mrefu tangu akiwa mdogo kabisa ameshiriki mafanikio mengi ya timu, mara baada ya kuleta maombi hayo sisi tulimkubalia na tunamtakia kila la kheri huko aendako katika maisha yake mapya,” alisema Idd.
Katika hatua nyingine Iddy alisema kocha wao mpya, Mholanzi Hans van der Pluijm atajiunga na klabu baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho Azam Sports Federation (ASFC) akiiongoza kwa mara ya mwisho klabu yake ya sasa Singida United.
Pluijm ambaye timu yake, Singida United kesho itamenyana na Mtibwa Sugar katika fainali ya ASFC, anakuja Azam FC kuchukua mikoba ya Mromania Aristica Cioaba, aliyekuwa na kikosi hicho msimu uliopita.
“Kwa sasa tumeamua kumtangaza baada ya kukubaliana naye kila kitu, mambo mengine tutayaweka wazi Jumatatu ijayo, na kingine kuanzia msimu ujao Azam FC itakuwa kampuni ikijulikana Azam FC Company Limited,” alisema Idd.
No comments