KLOPP AMKANYA SALAH TABIA HII.
LONDON, England
KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp, amemuonya winga wake, Mohamed Salah, kutoizoea tabia ya kujiangusha na kurudisha makali ya kufunga mabao kuelekea fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya kufunga mabao 11 katika mechi saba mfululizo, kwa sasa Salah amekumbwa na ukame wa mechi tatu bila kuziona nyavu na hali ilionekana kuwa mbaya zaidi dhidi ya Chelsea wikiendi iliyopita, alipoonekana kujiangusha ili kumhadaa mwamuzi.
Hata hivyo, Salah aliishia kuoneshwa kadi ya njano na kushuhudia timu yake ikikubali kichapo cha bao 1-0, kitendo ambacho kilimfanya Klopp aibuke na ushauri kuwa winga wake huyo anatakiwa kuacha tabia hiyo.
“Ndio, Salah alijiangusha au pengine alisubiri aguswe ndio aanguke lakini ni kitu nisichotaka kuona mchezaji wangu akikifanya,” alisema kocha huyo.
“Anatakiwa kuonesha kiwango bora, ninaamini atafunga tena. Mchezo wa leo (juzi) ulikuwa mgumu, hakupata nafasi kama ilivyo kawaida,” aliongeza.
No comments