Waamuzi wawili wang'olewa Ligi ya Mabingwa Mikoa SATURDAY MAY 12 2018
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewaondoa waamuzi wawili kwenye orodha ya Waamuzi wa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inayoendelea kwenye vituo vinne vya Geita, Singida, Rukwa na Kilimanjaro kutokana na uwezo mdogo wa kutafsiri sheria 17 za soka.
Waamuzi walioondolewa ni pamoja na Seleman Nonga kutoka Arusha aliyekuwa katika kituo cha Geita na Dadu Fadhil Msemo wa Kilimanjaro aliyekuwa kituo cha Singida.
Nonga ameondolewa baada ya kuonyesha kiwango hafifu cha uchezeshaji, kushindwa kumudu mchezo, kukosa umakini, kutozingatia sheria ipasavyo kwa kipindi kikubwa cha mchezo na kupata alama ndogo katika tathmini ya wasimamizi kwenye mchezo namba A7 kati ya Kumuyange FC dhidi ya Ambassador.
Msemo ameondolewa baada ya kuonyesha kiwango hafifu cha uchezeshaji, kushindwa kumudu mchezo,kukosa umakini, kutozingatia sheria ipasavyo kwa kipindi kikubwa cha mchezo na kupata alama ndogo katika tathmini ya wasimamizi kwenye mchezo namba C6 kati ya Temeke Squad dhidi ya Mtwivila City.
Hata hivyo, TFF imesisitiza haitawavumilia waamuzi watakaoendelea kuchezesha chini ya kiwango katika mashindano hayo ya RCL pamoja na mashindano mengine yote kwa kuwa imejielekeza katika uchezeshaji wa haki katika mashindano yake yote na haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayetaka kuharibu mashindano ya hayo.
No comments