MO APANGA MIKAKATI KUUA JS SAOURA
Dar es Salaam. Wakati Simba ikihesabu siku tu kabla ya kuanza kuonyesha makeke kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, mabosi wa klabu hiyo wakiongozwa na bilionea waoa, Mohamed Dewji ‘MO’ wameitana leo Jumamosi kwa ajili ya kuweka mikakati kuhakikisha timu yao inashinda mchezo huo.
Simba na JS Saoura zinacheza Jumamosi ijayo Januari 12 kwenye Uwanja wa Taifa, ikiwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Baada ya mpambano huo, Simba itakwenda DR Congo kuikabili AS Vita na kurejea nchini kuisubiri Al Ahly ya Misri Ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi hizo, mabosi wa Simba wakiongozwa na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji (Mo) wameitana ili kuweka mambo sawa sanjari na kupanga mikakati ya ushindi kwenye mechi hizo.
Mwenyekiti wa Simba, Swedi Mkwabi aliliambia gazeti hili jana kwamba, Bodi ya Simba inakutana jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine kikubwa watakachokijadili ni kuelekea kwenye mechi zao ma makundi Afrika wakianza na JS Saoura.
“Kikao hicho kitajadili vitu vingi, ikiwamo kupanga bajeti ya kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mechi zetu za makundi lakini kikubwa zaidi tunaiangalia mechi hii iliyopo usoni.
“Tutaweka mkazo hapa kwanza, tufanye nini, tutavuka vipi na kisha tutaangalia hizo mechi nyingine. Tutaweka mkakati na lazima ushindi upatikane,” alisema Mkwabi.
Alisema lengo la Simba ni kuhakikisha wanafuzu robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa au kusonga mbele zaidi ya hapo.
“Tuna amini timu yetu itafanya vizuri na kuweka rekodi hiyo, lakini pia kama uongozi inabidi kuweka mikakati mbalimbali ili tufanye vizuri,” alisema.
Wakati huo huo, Serikali imeahidi kuwaandalia Simba mazingira bora kwenye mechi zao za Ugenini watakapokwenda Algeria, Misri na DR Congo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo alisema watazungumza na balozi za Tanzania katika mataifa ambayo Simba itakwenda kwa ajili ya kuweka mambo sawa ikiwemo suala la usalama kwa wachezaji.
“Hawa wanatuwakilisha, lazima Serikali iweke mazingira bora watakapokuwa ugenini kwenye mechi zao za Ligi ya Mabingwa,” alisema.
Mchambuzi wa Soka nchini na nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema ushauri wake kwa viongozi wa Simba kwenye kikao cha leo wahakikishe wanawaandalia mazingira mazuri wachezaji kuelekea kwenye mechi zao za makundi.
“Waandae bajeti ya kutosha, lakini kikao hicho kisijekuishia kuwapa presha wachezaji, viongozi waanze kuiona kama mechi hiyo ni ya kawaida kuliko kutoa maagizo mengi mengi yakawachanganya wachezaji na hata kuiona kama mechi ya presha, hiyo itawaathiri wachezaji, “alisema Mayay.
Nyota wa zamani wa Simba, Mtemi Ramadhani ambaye alifunga bao la pili Simba ikiiua Al Ahly ya Misri 2-1 mwaka 1986, alisema miongoni mwa mambo ambayo anadhani uongozi wa Simba ufanye ni kucheza mechi yao na JS Saoura saa 9:00 alasiri.
“Kule kwao ni baridi kali, hivyo hiyo itawaathiri labda mvua inyeshe, lakini pia kuweka kiingilio kidogo ili kuwahamasisha mashabiki waingie kwa wingi kama siku na Nkana.
“Pia katika mikakati yao, mbali na ushindi, kuhamasisha mashabiki wao kuujaza uwanja wa Taifa na mwisho waiandalie timu mazingira ya kufanya mazoezi ya nguvu kwa siku zilizosalia.
No comments