KAKOLANYA NDIO BASI TENA
WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera akisisitiza kutomtambua kipa Beno Kakolanya, meneja wa mchezaji huyo Haroub Seleman, amesema wako kwenye mchakato wa kutumia sheria kumaliza suala hilo.
Lakini, kwa upande wake uongozi wa Yanga kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu, Omary Kaya, umeweka wazi kuwa Kakolanya aliandika barua kuvunja mkataba wake na klabu hivyo, milango iko wazi kuondoka ila afuate taratibu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaya alisema Beno aliiandikia Yanga barua ya kuomba kuvunjiwa mkataba na wakati wakitafakari cha kufanya walipokea barua nyingine kutoka kwa meneja wake, jambo lililoashiria kuwa Kakolanya haitaki Yanga.
"Tuna barua ya kuvunjwa kwa mkataba na hatuna sababu ya kujibu na ishu ya Benno kutaka majibu halina maana, tayari yupo huru kwa kile alichoandika kwa uongozi anaruhusiwa kutafuta timu ili taratibu zingine zifuate," alisema.
Kaya alisema ishu ya kuondoka ni uamuzi wa Beno hivyo, hawana sababu ya kufanya majibizano na ndio sababu wako kimya wakiendelea na harakati za kutafuta ubingwa na sio vinginevyo.
Lakini, wakati Yanga wakiweka msimamo huo, Seleman amesema wamefanya jitihada zote za kumrudisha mchezaji wake kikosini bila mafanikio hivyo, wanatafuta wanasheria kwa ajili ya kupata msaada.
Alisema suala la Benno lipo kisheria zaidi hivyo, watatafuta msaada ili waweze kulisimamia hilo na kuhakikisha mwafaka unapatikana.
KAKOLANYA AFUNGUKA
Kakolanya, ambaye hajaichezea Yanga tangu mwezi Novemba baada ya kurejea kutoka kwenye majukumu ya timu ya Taifa, Taifa Stars, akishinikiza kulipwa mshahara na pesa usajili wake, alisema aliuandikia uongozi barua kwa ajili ya kuwakumbusha vipengele vilivyopo katika mkataba wake.
Alisema kuwa aliomba kuvunjwa kwa mkataba wake kutokana na kutolipwa mshahara kwa zaidi ya miezi mitatu, lakini tangu wakati huo uongozi umekaa kimya bila kumjibu.
Hata hivyo, amesema kuwa licha ya kutocheza bado ni mchezaji halali wa Yanga kwa mujibu wa mkataba wa miaka miwili ambao, amesanishwa na uongozi.
"Mimi bado ni mchezaji wa Yanga kwa mujibu wa mkataba wangu, sipo kikosini kutokana na matatizo yaliyotokea lakini bado naendelea kufanya mazoezi mwenyewe ili kulinda kipaji changu nisiondoke mchezoni.
"Bado natamani kuendelea kuichezea Yanga hata nikipewa nafasi leo nitarudi kufanya kazi kwa sababu nina mkataba ambao, unanitambulisha kama mchezaji,” alisema.
AMUNIKE AMREJESHA YANGA
Kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Emmanuel Amunike, ameibuka baada ya kusikia sekeseke la Kakolanya kusimamishwa kuitumikia klabu yake.
Kakolanya amekuwa akiitwa mfululizo katika kikosi cha Stars, tangu enzi za Salum Mayanga na sasa ikiwa chini ya Amunike.
Amunike aliliambia Mwanaspoti kuwa, alikuwa hafahamu kama Kakolanya alisimamishwa lakini alimshauri kurejea katika kikosi chake ili aweze kupata nafasi ya kuitwa tena katika kikosi cha timu ya Taifa.
“Beno ni kipa mzuri akiwa katika klabu yake hata timu ya Taifa, napenda kumuona akicheza ili kukuza kiwango chake. Mchezaji akiwa hachezi ni jambo bay asana kwenye timu kwa sababu linaiweka nafasi yake katika timu ya taifa mahali pabaya,” alisema.
“Sipendi kuzungumzia mambo ya Yanga kwa sababu maamuzi yamefanywa na kocha wake na sijui tatizo hilo kiundani, lakini ninachotambua Kakolanya ni mchezaji wa Yanga na timu ya Taifa kwa kipindi hiki,” alisema.
Amunike hivi sasa yupo nchini Hispania ambapo ndio makazi yake yalipo, anatarajia kuingia nchini kuanzia Januari 10 kwani Januari 8 atakuwa katika tuzo ya mchezaji bora wa Afrika itakayofanyika Januari 8, Senegal.
No comments