Breaking News

GORMAHIA YAJIPINGIA YANGA KIULAINI TAIFA



Yanga imepoteza mchezo wa pili dhidi ya Gor Mahia kwenye michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya leo kukubali kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa mabingwa hao wa Kenya.

Makosa ya mlinda lango Youthe Rostand yameigharimu Yanga katika mchezo huo muhimu ambao ilihitaji kuibuka na ushindi.

Gor Mahia ilianza kuhesabu bao la kwanza kwenye sekunde ya 33 mfungaji akiwa George Odhiambo.

Bao la pili lilifungwa na Jaques Tuyisenge likiwa ni zawadi kutoka kwa Rostand aliyefanya makosa ya kuokota mpira uliomponyoka akiwa ndani ya eneo la hatari. 

Tukio hilo lilipelekea mwamuzi kuwapa Gor Mahia mpira wa adhabu ndani ya eneo la hatari la Yanga na Tuyisenge kuukwamisha mpira wavuni.

Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 2-0. 

Kipindi cha pili Yanga ilirejea ikiwa na nguvu ya kusaka mabao ya kusawazisha na ilifanikiwa kufunga bao la kwanza kwenye dakika ya 59 mfungaji akiwa Deus Kaseke aliyemalizia mpira iuliotemwa na mlinda lango wa Gor Mahia.

Hata hivyo bao hilo halikudumu kwani kwenye dakika ya 64 Haruni Shakava aliifungia Gor Mahia bao la tatu.

Kocha Mwinyi Zaherav ambaye alikaa kwenye benchi la ufundi kwa mara ya kwanza alifanya mabadiliko kwenye kipindi cha pili kwa kuwaingiza Ibrahim Ajib na Juma Mahadhi wakichukua nafasi za Yusufu Mhilu na Deus Kaseke huku pia akimtoa Rostand kwenye dakika ya 75 na nafasi yake kuchukuliwa na Benno Kakolanya.

Mashabiki wa Yanga walishangilia kutolewa kwa Rostand ambaye uzembe wake ulipelekea Gor Mahia kufunga mabao mepesi.

Kwenye dakika ya 81 Raphael Daudi aliifungia Yanga bao la pili akimalizia mpira uliotemwa kwa mara nyingine na mlinda lango wa Gor Mahia.

Matokeo hayo yameondoa matumaini ya Yanga kusaka moja ya nafasi za kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

No comments