Breaking News

MATOKEO LIGI RUVU YAANGUKIA PUA

WAKATI Ruvu Shooting ikipapaswa kinyonge kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza kwa kufumuliwa mabao 3-0 na Alliance, Kocha Amri Said 'Jaap Stam' ameanza kazi kwa mkwara akiandika rekodi Biashara United katika Ligi Kuu Bara.

Biashara ilikuwa haijawahi kupata ushindi kwenye Uwanja wao wa nyumbani tangu wapande Ligi Kuu msimu huu, lakini jioni hii iliicharaza Mbeya City kwa mabao 2-1 na kuandika ushindi wao wa pili katika ligi hiyo.

Mabao ya Daniel Manyenye na Juma Mpakala yalisaidia kumfanya Stam kuanza kibabe kazi ya kuinoa timu hiyo akitokea Mbao FC ya jijini Mwanza. Bao la Wagonga Nyundo wanaouguza kipigo cha pilio mfululizo baada ya wikiendi kufumuliwa na Yanga 2-1 liliwekwa kimiani na Frank Ikobela likiwa ni bao la kuongoza kwenye mchezo huo.

Katika michezo mingine, Lipuli ikiwa nyumbani iliwatambia Prisons inayonolewa na Kocha Mohammed Rishard 'Adolph' kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa. Bao hilo lililowapa alama tatu muhimu Lipuli liliwekwa kimiani na Jimmy Shoji.
Nao Stand United ikiwa Uwanja wa Kambarage, Shinmyanga waliicharaza JKT Tanzania kwa bao 1-0 lililowekwa wavuni na Morrice Mahela dakika ya 73, huku Singida United ikibanwa nyumbani mjini Singida na Wagosi wa Kaya,  Coastal Union kwa kutoka nao sare ya bao 1-1, huku winga Geofrey Mwashiuya akifunga bao lake lwa kwanza msimu huu katika dakika ya 64' akisawazisha bao la Coastal la Mbwana Bakar  aliyefunga dakika ya 58. Kagera Sugar na Mbao walishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, pia jijini humo, Ruvu walishindwa kuhimili vishindo vya madenti wa Alliance kwa kulala mabao 3-0, huku Hussein Javu, Dickson Ambundo na Bigirimana Blaise wakitupia kambani mabao hayo na kuipa ushindi timu yao iliyopanda msimu huu

No comments